Monday, September 23, 2013

Uvaaji wako unaathiri kinyota?


By on 5:38 AM

Sikuweza kuelewa kwa haraka, lakini ilinishangaza sana pale mzee mmoja wa kihindi aliponiambia; "hiyo pete yako haikufai, tafuta pete ya dhahabu na iwe na jiwe la 'saphire'".

Sikuwa namfahamu mzee huyu, nilikutana naye kwa bahati nilipokuwa kwa rafiki yangu mmoja wa kihindi mitaa ya Kariakoo, na maongezi yake yalinistusha kidogo.

Pete niliyokuwa nimevaa ni ya madini ya fedha, nimekuwa nikivaa pete hii kwa takribani miaka miwili sasa, sijawahi kuona tatizo lolote lililoletwa na pete hii, kwa hiyo kauli yake ilinishangaza na ilibidi nimuulize rafiki yangu; "huyu mzee vipi?"

Rafiki yangu alinieleza kuwa huyu mzee ni mtabiri wa nyota, kwamba kwa muda mwingi amekuwa akifanya kazi zake katika jamii ya wahindi hapa mjini na kuwa imekuwa kama bahati kwangu kukutana naye na kunieleza mambo hayo.

Huwa siamini masuala ya nyota, lakini kwa muda mchache uliofuata baada ya mazungumzo na mzee huyo wa kihindi nilianza kuhisi kama naanza kubadilika kimawazo, nikaanza kuamini kidogo masuala hayo.
Kwa tarehe yangu ya kuzaliwa na mwezi, Novemba 24, mzee yule aliniambia kuwa nyota yangu ni mshale, hilo halikunishangaza kwa sababu nalijua siku nyingi, lakini alichonieleza ambacho sikuwa nakijua, ni mambo mengine ya watu wa nyota hiyo.

Alinieleza mambo mengi ya watu wa 'mshale', ambayo kwa hakika mengi yalikuwa yanafanana na mambo yangu binafsi, akanieleza na tabia za watu wa nyota yangu, ambayo nayo yalikuwa karibu sawa na tabia zangu.

"Wewe una tabia ya kuwa na matumaini kuwa utafanikiwa kwa jambo lolote unalofanya au unalotegemea kupata," alisema mzee huyo na kuendelea; "unapenda kuwa na uhuru wa kufanya mambo yako hata kama watu watakuambia kuwa jambo hilo ni baya na unapenda watu wengine wawe kama wewe".

Mzee huyu aliendelea kunieleza kuwa mimi ni mtu nisiyependa kuamrishwa kufanya jambo kwa sababu naamini kuwa nina uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote; "na ukiudhiwa unakuwa mkaidi na hutii amri ya mtu yoyote", alisema.

Kwa mujubu wa elimu yake, mzee huyu alisema; "hali hiyo inasababishwa na mtawala wa nyota yako, ambayo ni moto, moto ni kitu kizuri kwa watu, lakini watu wanapoutumia vibaya moto huwa na madhara kwao, lazima utaleta hasara."

Kwa muda mzee huyu aliendelea 'kunichambu' kwa jambo moja baada ya jingine, akasema; "katika mapenzi, kwa nyota yako wewe ni mtu ambaye unapoanzisha uhusiano unakuwa ni mwaaminifu, lakini kinyota unapenda kila wakati kuwa na wapenzi wapya au mapenzi ya kawaida, sio ya kudumu, kwa sababu unaona mapenzi ya kudumu yakunyima uhuru."

Kwa kuona hali yangu ya kushitushwa na mazungumzo hayo, mzee huyu wa kihindi ambaye mida wote alikuwa akitabasamu, aliwahi haraka kunieleza kuwa; "hii ni nyota tu baba, unaweza kujibadili ukipenda".

Inawezekana kuwa na wewe ni mtu wa nyota ya mshale kama mimi, ikiwa hivyo unaweza kuchukuwa maneno ya mzee huyu kama changamoto kwako na kujichunguza kitabia kuona kama yanaendana na wewe.

Kwa upande wa kazi, mzee huyu alisema; "kwa nyota yako wewe unatakiwa kufanya kazi za kusafiri safiri hivi, kazi za sheria; uwakili au uhakimu, kazi za uandishi, ualimu, kazi za kidini; uwe sheikh au padri au kazi zozote za makanisani au misikitini, kazi za michezo, kazi za kijeshi na biashara hasa ya kuuza vitu."

Pia hakuacha kunichagulia mavazi, alisema; "kwa nyota yako wewe unatakiwa kuvaa mavazi ya
nguo zenye zambarau au rangi ya kahawia iliyochangamka au rangi ya blue na ziwe za vitambaa vya sufu na zimeshona kiutamaduni kwa kuchanganya rangi au ukivaa koti na suruali basi zisiwe katika mpangilio wa rangi moja, ziwe za kuchekesha chekesha hivi".

Niliuliza; "kwa wanawake wa nyota hii nao je, wanatakiwa wavae mavazi gani?" nikajibiwa kuwa sketi na blauzi ni mavazi mazuri kwao na rangi zao ziwe hizo na siku za nzuri kwa watu wote wa mshale ni Alhamisi na namba yao ya bahati ni namba tatu.

Baada ya kupata utabiri huo, wa bure, nilishawishia kutaka kujuwa kama kuna watu wengine wanaovaa nguo au vito huku wakijua ni nini athari au maana ya kuvaa vito hivyo? Utafiti wangu nilifanya zaidi kwa watu ambao walikuwa wamevaa pete zenye vitu maalumu.

Mzee Sadiq Izunya, mkazi wa Kariakoo, yeye anavaa pete yenye kito cha marijani, anasema; "ni kweli pete hizi tunazivaa kwa maana, mimi nilikuwa na maradhi mabaya ya nyonga, nimejaribu kutibiwa sehemu mbalimbali lakini sikupa nafuu, ila bwana mmoja 'mtaalamu' alinishauri nivae pete hii na kutumia dawa nikapona."

Kama mzee Izunya, watu wengi niliowakuta na pete zenye vito walizieleza pete hizo kuwa zina maana maalum, wengi wao wakiwa wamevaa kwa ushauri wa waganga au wengine kwa imani ya masuala ya nyota.

Katika utafiti huo mdogo, niligundua pia wapo watu ambao huamua kuweka vito hivyo baada ya kushauriwa na masonara ambao wao huwa na orodha ya aina za vito kwa mujibu wa nyota za watu.

Katika hali hiyo, ya kufuata nyota kwa vito kwa kuzingatia alama zake, inashauriwa na wataalam wa masuala hayo mtu asipende kuvaa kito bila ya kujua maana yake au nini madhara ya kito hicho kwa upande wa nyota yake, lakini inawezekana pia kuwa jambo hilo ni sahihi au si sahihi.

About Syed Faizan Ali

Faizan is a 17 year old young guy who is blessed with the art of Blogging,He love to Blog day in and day out,He is a Website Designer and a Certified Graphics Designer.

5 comments:

  1. Kama nataka nyota zangu zirudu zilizochukuliwa nifanye nini maisha yangu yamekufa

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nipigie sim usijali nitakuludishia na nyingine nitakupa ukizitaji

      Delete
    2. Utajuaje kuwa nyota yako imechukuliwa

      Delete
  2. Mi nataka unielekeze kw uyo mzee

    ReplyDelete
  3. Kwahiyo sisi wa mshale tuvae vito vyenye rangi gani

    ReplyDelete