Tuesday, September 24, 2013

Azam TV itakavyohatarisha utawala Simba na Yanga


By on 11:25 PM

Kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom haijaanza, Kamati ya

Ligi ilikuwa kwenye mchakato wa kutafuta mdhamini wa kuonesha moja kwa moja ‘live’ Ligi hiyo, ambapo Kampuni za Multichoice kupitia Kituo chake cha Supersports na Kampuni ya Azam Media kupitia Azam TV, walijitokeza kutaka kupewa nafasi ya kumiliki haki za matangazo hayo ya ligi.

Azam Media ambayo ndiyo imeanzishwa mwaka huu, ilishinda katika mchakato huo na kufanikiwa kupata haki za kuonesha ‘live’ ligi hiyo, ambapo walisaini mkataba wa kudhamini ligi kwa misimu mitatu ijayo wakianza na msimu huu.

Mkataba uliogharimu Sh bilioni 5.6 kwa misimu yote ya udhamini huo.

Mpaka sasa klabu 13 za ligi hiyo, zimeshapokea sehemu ya fedha za awali kutoka Azam TV kwa ajili ya udhamini wa msimu huu, ambapo kila timu imepewa milioni 25, huku zikibakia milioni 75 ambazo watapewa miezi miwili ijayo, kwani kwenye msimu huu kila timu zitapokea Sh milioni 100.

Klabu ya Yanga bado haijapewa fedha hizo, baada ya klabu hiyo kupinga udhamini huo, wakidai itawafanya mashabiki wao kutokwenda kwa wingi uwanjani katika mechi zao, kwani wanategemea kwa kiasi kikubwa fedha za milangoni kwenye uendeshaji wa klabu.

Hivi sasa wapo kwenye mazungumzo na kampuni hiyo kufanya makubaliano mengine nje ya udhamini huo, ambayo yatawaingizia fedha za ziada.

Msimu uliopita, klabu za ligi hiyo zilitaka kumgomea mdhamini wa ligi, Kampuni ya Vodacom kutokana na kipengele cha kutoruhusu mpinzani wake (kampuni nyingine ya mawasiliano ya simu za mkononi), kuingia udhamini na klabu hizo, lakini baadaye walikubali kucheza wakiheshimu sheria za soka na pia mkataba wa kampuni hiyo.

Ligi hiyo imefikia raundi ya tano hivi sasa, ambapo tumeshuhudia upinzani mkali unaooneshwa na timu zote, hasa baada ya kuchagizwa na udhamini mnono wanaoupata kwa wadhamini wa Ligi hiyo, Vodacom na Azam TV.

Klabu zote zimefanya usajili mzuri na pia udhamini umewasaidia kuziandaa vyema timu zao na hawana matatizo mengi ya kifedha kama yaliyokuwa kipindi cha nyuma wakati ligi ikiwa na mdhamini mmoja pekee.

Klabu kongwe za Simba na Yanga, zilikuwa zinatawala soka nchini kwa kuzionea timu ndogo kila msimu, lakini msimu huu hali ni tofauti, kwani timu hizo zimecheza mechi mbili viwanja vya mikoani, Simba imeambulia pointi nne pekee kati ya sita huku ya Yanga ikiambulia pointi mbili pekee.

Hata kauli za makocha na viongozi wa timu hizo, wamekiri msimu huu si mchekea kama ilivyo kipindi cha nyuma, wakisema wamekuwa wakikamiwa sana na timu mbalimbali wanazocheza nazo kwenye mechi za ligi, hasa wakihofia viwanja vya mikoani.

Kocha Juma Mwambusi anayeifundisha timu ngumu ya Mbeya City, amefanikiwa kuzikaba koo timu hizo katika mechi alizokutana nao, akiibana Yanga kwa sare ya 1-1 na pia Simba kwa sare ya 2-2, huku Simba ikiwa mbele ya mashabiki wake waliojazana katika Uwanja wa Taifa.

Pia hata klabu nyingine za Azam na Coastal Union ambazo zina wachezaji wa gharama kubwa, nazo zimekuwa zikionja ugumu wa ligi hiyo, ambayo imefikia robo ya msimu hivi sasa.

Ukiangalia kwenye msimamo wa ligi mpaka hivi sasa, utagundua ugumu ninaouzungumzia hapa, kwani ukianzia kwa Simba inayoongoza Ligi hiyo, timu zimepishana pointi mbili kimsimamo na timu yoyote inayoshinda mchezo wake hujikuta imepanda sana kwenye msimamo.

Hali hii ndiyo ilikuwa inatafutwa kwa muda mrefu katika mapinduzi ya soka letu na kwa hakika utawala wa Simba na Yanga utapotea kadiri misimu itakavyokuwa ikienda mbele.

Kwani muda mfupi ujao tutashuhudia timu zikipata udhamini mwingine binafsi na ule wa wadhamini wa ligi, ambao utaongeza ugumu zaidi ya huu tunaoushuhudia hivi sasa.

Klabu ya Ashanti United imeshaanza kuneemeka mapema, hasa baada ya Kampuni ya Bakhresa, kuwapa udhamini wenye thamani ya Sh milioni 35 kwa ajili ya msimu huu.

Kwa hakika mapinduzi yameanza kuonekana na kikubwa ni fahari kwa nchi yetu, kwani itachochea maendeleo ya mchezo huu na kufikia kule wenzetu walipoendelea na yote hayo yamesababisha na timu zote kujiweza kifedha kupitia udhamini walioupata.

About Syed Faizan Ali

Faizan is a 17 year old young guy who is blessed with the art of Blogging,He love to Blog day in and day out,He is a Website Designer and a Certified Graphics Designer.

0 comments:

Post a Comment