Monday, September 23, 2013

Mbeya City yaisimamisha Simba SC


By on 1:28 AM

Timu ya Simba SC imelazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbeya City, katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Licha ya sare hiyo

, Simba inaendelea kuongoza ligi kwa kufikisha pointi 11.

Simba walianza kufanya mashambulizi langoni mwa Mbeya City katika dakika za mwanzo, lakini katika dakika ya 27, mshambuliaji anayekuja juu kwa kupachika mabao katika ligi hiyo, Amis Tambwe, aliwainua mashabiki wa timu hiyo baada ya kufunga bao la kwanza, baada ya kuuwahi mpira uliomshinda kipa wa Mbeya City, David Baruani, kutokana na shuti lililopigwa na William Lucian.

Tambwe aliiandikia Simba bao la pili katika dakika ya 33, baada ya kumalizia krosi ya Haruna Chanongo na sasa kuwa mchezaji pekee anayeongoza kwa upachikaji mabao akifikisha mabao 6.

Mbeya City ambao wameonekana kuwa tishio katika ligi msimu huu, walikuja juu na kupata bao la kwanza katika dakika ya 36, kupitia kwa Paul Nonga, aliyemalizia pasi ndefu ya Deogratius Julius.

Kipindi cha pili Mbeya City, inayonolewa na Kocha Juma Mwambusi, ilijiimarisha vema kwa kufanya mabadiliko katika dakika ya 60, kwa kumtoa Mwigane Yeya na kuingia Richard Peter.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Mbeya City, kwani katika dakika ya 67, Richard Peter, alimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Antony Matogolo.

Baada ya kusawazisha, Mbeya bado waliendelea na kasi yao ile ile, waliyoingia nayo uwanjani, huku Simba wakionekana kuchoka kidogo, ambapo walifanya mabadiliko kwa kumtoa Amri Kiemba na kumuingiza Ramadhani Singano.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuwa na tija, kwani hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zikitoka sare ya mabao 2-2.

Naye Oscar Assenga, anaripoti kutoka kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuwa timu ya Mgambo JKT imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora. Bao la Mgambo lilifungwa katika dakika ya 60 kupitia kwa Malimi Busungu, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Salim Aziz. Rhino walisawazisha bao hilo katika dakika ya 89 kupitia kwa Hamis Msafiri.

Kutoka Mbeya, Upendo Fundisha anaripoti kuwa timu ya Prisons imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wake wa Sokoine. Mtibwa walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 26, lililofungwa na Shaaban Nditi, huku Prisons wakisawazisha katika dakika ya 53 kupitia kwa Peter Michael.

Naye Mwandishi Wetu kutoka kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba anaripoti kuwa Kagera Sugar imeinyuka Ashanti United mabao 3-0.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa mabingwa watetezi wa taji hilo, Yanga kucheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, wakati JKT Ruvu wao wataikaribisha JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku Coastal Union ikiwaalika Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

About Syed Faizan Ali

Faizan is a 17 year old young guy who is blessed with the art of Blogging,He love to Blog day in and day out,He is a Website Designer and a Certified Graphics Designer.

0 comments:

Post a Comment