Hivi sasa gumzo katika Ligi Kuu ya Vodacom ni kitendo cha mwamuzi Jacob Adongo, aliyechezesha mechi ya Simba na JKT Mgambo Shooting, kumnyima mpira mchezaji wa Simba,
Kitendo hicho kimepingwa na wadau wa mchezo huo nchini, ambao wamesema kitendo hicho si cha kiungwana, kwani mchezaji anayefunga ‘hat trick’, lazima apewe heshima yake ya kuondoka na mpira uwanjani.
Katikati ya wiki hii, kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, tulishuhudia wachezaji Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakipewa mpira kila mmoja na waamuzi waliochezesha mechi za timu zao, baada ya kufunga ‘hat trick’.
Msimu huu tumeshuhudia ushindani wa kweli kwa asilimia kubwa kwa timu za ligi kuu nchini.
Ushindani huo umesababisha timu za Simba, Yanga, Azam, Coastal Union na Mtibwa Sugar zihofie kila zinapoteremka dimbani kwenye mechi zao mbalimbali, hasa kutokana na namna timu ndogo zilivyojipanga.
Mwanzoni mwa ligi hiyo, tulishuhudia Simba ikibanwa mbavu kwa sare 2-2 na timu ya Rhino Rangers ya Tabora, pia kwenye raundi ya nne Azam FC nayo ilibanwa kwa sare ya 1-1 na Ashanti United, iliyopanda daraja.
Ugumu wa vigogo kupata matokeo haukuishia hapo, kwani Yanga iliyokuwa jijini Mbeya, iliweza kuambulia pointi mbili pekee katika mechi mbili na timu za huko, wakitoka sare ya 1-1 na Mbeya City na sare kama hiyo hiyo dhidi ya Tanzania Prisons.
Huo ni mwanzo wa ligi, kwani ni raundi tano pekee zimechezwa mpaka sasa, hakika imeonesha ishara nzuri na mwishoni mwa msimu huu tunatarajia kupata matunda mazuri, ambayo yatapelekea kuimarika kwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Pia ushindani huu unatarajia kuongezeka maradufu, baada ya Azam TV kuanza kurusha mechi za Ligi moja kwa moja ‘live’, ambapo wamepanga kuanza urushaji huo mwezi ujao.
Kuonekana ‘live’ kutawafanya wachezaji kuongeza juhudi na kuonesha viwango vya hali ya juu, wakiwa na lengo la kutafuta soko kwa timu nyingine kubwa nchini na nje ya nchi, hivyo tutashuhudia Ligi ngumu na yenye ushindani kupita ilivyo sasa.
Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen, yupo kwenye mawindo ya kusaka wachezaji wapya katika mikoa mbalimbali atakaowaongeza katika timu hiyo.
Safari za Kim mikoani kushuhudia mechi hizo zitazaa matunda mazuri, kwani atapata wachezaji wazuri wa kuziba mapengo katika kikosi chake cha hivi sasa, hasa kutokana na ushindani unaooneshwa na wachezaji wa timu za ligi hiyo.
Inshaallah! Tutashuhudia Stars mpya yenye wachezaji waliopikwa vyema kwenye Ligi ya ushindani, ambao wataleta changamoto mpya na kuanza vyema safari yetu ya kuelekea AFCON 2015 nchini Morocco na Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

0 comments:
Post a Comment