Uvimbe mweusi unaoonyesha kuvilia kwa damu ulikuwa karibu na jicho lake, chini kidogo ya jicho la mkono wa kushoto, hali hii ilionyesha kuwa alipatwa na dhoruba fulani, na rangi yake ya 'mkorogo' ilizidisha athari kwenye uvimbe ule na kuonyesha hali ya 'hatari'.
"Vipi, imekuwaje?", alimuuliza rafiki yake ambaye ndiye niliyekuwa naye.
"Mwenzangu we acha tu!", alisema yule mwanamke mwenye 'ngeu' na kuongeza; "hawa wanaume wengine watatuua".
"Usiniambie kuwa shemeji kakupiga tena", akadadisi yule mwenzake ambaye sasa sauti yake iliyojaa huruma ilikuwa na shauku ya kujua kwa uhakika ni nini kimepata mwenzake.
"Ndio huyo huyo," akajibu yule mwanamke.
Kilichofuata ni hadithi ndefu ya kisa cha kipigo alichopata mwanamke yule, alieleza kuwa mpenzi wake alimpiga baada ya yeye kuacha kupokea simu yake na alipoenda nyumbani kwake hakumkuta, na kwa maneno ya mwanamke huyo ni kwamba siku hiyo alikuwa na mashoga zake kwenye dansi la bendi moja maarufu.
Kwa 'hesabu' za harakaharaka, mtu anaweza kusema kuwa mpenzi wa mwanamke huyu hakuwa na sababu za kumpiga na kumuumiza mpenzi wake kiasi hicho, kwenda dansi na mashoga zake tu iwe sababu ya kumpiga kiasi hicho?
Lakini, 'ukipiga hesabu' nyingine, utaona kuwa mwanamke yule naye alikuwa na kosa, iweje aende dansini bila ya kumuaga mpenzi wake? Na kwa nini pia asipokee simu yake wakati alipompigia? Inawezekana kuna jambo alilolificha na ndilo lililomfanya mpenzi wake kumuangushia kipondo kile.
Nilipoachana na mshaoga wale, akili yangu ikazunguuka na kujiuliza hivi ni kwa nini mtu kama kweli anampenda mwenzie anafikia hatua ya kumpiga na kumumiza kiasi kile? Kweli katika mapenzi halisi, ambayo watu wanaheshimiana na kuthaminiana inawezekana kutokea kupigana?
Ili kupata majibu ya maswali haya, niliamua kuzungumza na watu kadhaa ambao nao wana mitizamo tofauti katika hili."Kiukweli katika mapenzi ya kweli na ya dhati kupigana ndio mahali pake," anasema Bi. Subira Gumbo mkazi wa Ilala Mchikichini, Bi, Gumbo anafafanua:
"Unajua saa nyingine katika mapenzi watu huwa wanatafuta 'bima' fulani ya kuhakikisha kuwa penzi lake kwa mwenzie liko salama na linaulinzi wa kutosha, kumkera mwenzio kwenye jambo ambalo unajuwa kabisa hawezi kulivumilia ni moja ya njia za kupata uhakika wa bima yako.
"Unapomtia kwenye majaribu ya wivu na ukaona kuwa amekasirika na anamua kukupiga basi hapo unapata uhakika wa bima yako kwamba penzi lako liko salama, lakini ukifanya kitu cha namna hiyo na ukaona kuwa ametulia tu, basi juwa kuwa wewe huna thamani ya mapenzi ya kweli kwake. Sie wanawake tunapenda kujaribu mambo namna hiyo, tunatafuta uhakika tu".
Inawezekana, kwamba ni kweli wanawake wengi wanaoanzisha chokochoko kwa wapenzi wao huwa wanatafuta uhakika kama kweli 'bima' yao ya mapenzi iko salama, lakini je wanaume wanalifahamu hilo? Na kama wanalifahamu wanalichukulia vipi?
"Aise linakera sana," anasema Bw. Adrean Ulaya, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam na kuendelea; "unajua wanawake ingawa ni mama zetu, dada zetu na wapenzi wetu, lakini wanakera sana".
Bw. Ulaya anatoa mfano wa mke wake wa kwanza, anasimulia; "yeye alikuwa ni mwanamke mzuri na mwaminifu, lakini tatizo lake lilikuwa moja, lazima katika wiki moja atatafuta sababu mpaka nimpige, angalau kidogo tu, na nikishampiga basi siku hiyo mapenzi yake kwangu yanakuwa kama ndio yameanza leo, atakuwa mwanamke mwema kuliko unavyodhani".
Bw. Ulaya anatoa mfano wa vituko vya mke huyo ambaye bahati mbaya alifariki wakati wa uzazi kuwa; "saa nyingine alikuwa anaweza kumwaga mchele kwenye zuria au akatawanya vitu sebuleni huku akijuwa kabisa kuwa kuna wageni watakuja, ukimuuliza kwa nini anafanya hivyo atakujibu jeuri ya ajabu, na ukimpiga, hata kofi moja tu, basi atatuliana na kufanya vitu vyote kwa mpangilio wake. Ajabu kabisa!".
Ni kweli, haya ni maajabu, mtu kuchokoza ugomvi kwa makusudi, hili ni ajabu kabisa! Lakini si kwa wanawake tu wenye tabia hii ya kutaka 'kuchokoza', wapo pia wanaume wanaodaiwa kuwa na tabia hiyo ya kuchokoza lakini wao ikiwa kwa kusudi la kupiga.
"Kuna wanaume wengine bwana wakorofi," anasema Bi. Lulu Dihule, mkazi wa Kimara Temboni, jjijini Dar es Salaam.
Bi. Dihule anatoa mfano kwa kusema; "utakuta mwanaume anarudi nyumbani kanuna, ukimuuliza mwenzangu vipi au hata kabla hujamuuliza atakuambia 'we na fulani mnajuani vipi?', utashangaa huyo fulani mwenyewe anayekuulizia labda ni mpangaji mwenzio au jirani yake, lakini akili zake za wivu tu zimemtuma akufikirie mambo mabaya na ukimjibu anakupiga".
Mikasa na visa vinavyoelezewa katika suala hili vyote vinadondokea kwenye wivu wa mapenzi, na hakuna neno zuri au tafsiri nzuri ya kuielezea kama neno alilolitumia Bi. Gumbo, kwamba wote wenye tabia hii wanatafuta uhakika wa 'bima' yao katika mapenzi, kwamba iko hai au imekufa.
Lakini, kwa Bw. Rashid Mujuni, mtabiri mchanga katika masuala ya nyota na unajimu, yeye analielezea vingine jambo hilo, anasema; "mara nyingi kupigana kwa wapenzi wanaopendana kidhati kunatokana na mchanganyiko wao kinyota".
Bw. Mujuni anafafanua; "kwa mfano watu wa nyota ya punda, hawa ni watu wakorofi katika mapenzi, ingawa kiasili ni watu wakarimu kwenye urafiki wa kawaida, na ukorofi wao katika mapenzi unatokana na tabia yao ya kupenda kupita kiasi, kwa hali hii wanatafuta sana uhakika kama wanaowapenda wanamapenzi kama ya kwao.
"Sasa inapotokea kutokuwa na uhakika na hilo, basi hugeuka na kuwa washari, wanapenda kuanzisha mambo mabaya ili waone kama kweli wapenzi wao wanawapenda kidhati, na uhakika wao kwa hilo ni kupigwa angalau kidogo tu, si mpaka uwaumize sana kwa sababu pia ni wepesi wa kubadilika na kuvutika kwa wapenzi wapya."
Inawezekana kuwa ni kwa sababu ya kutafuta uhakika wa 'bama ya penzi' au inawezekana pia ikawa kwa sababu ya athari za kinyota, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa katika penzi la kweli kupigana kunaongeza aina fulani ya chachu ya penzi kwa sababu wale wanaopigana mara nyingi si rahisi kuachana, wana 'mapenzi sugu'.
Hata hivyo, kwa sheria zote za serikali dunia nzima, kupigana kwa aina yoyote ile ni kosa mbele ya sheria na wenye kufanya hivyo wanaweza kushitakiwa chini ya sheria hiyo.

0 comments:
Post a Comment