Wiki iliyopita niliahidi kuiendeleza hoja niliyoiandika wiki iliyotangulia kuhusiana na mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kichwa cha makala ile kiliwafa
nya wasomaji wengi wanielewe vibaya kwa kuhoji kwa nini Kigamboni isijengwe Dodoma, wapo baadhi ya watu waliodhani kuwa ninaupinga mradi wa Kigamboni. La hasha, siupingi mradi huo hata kidogo.
Niliamua kuendelea na hoja hiyo kutokana na ujumbe mfupi wa maandishi na simu nilizopokea kutoka kwa baadhi ya wasomaji hasa mmoja ambaye alizungumza nami kwa takribani dakika 15, akijitahidi kunishawishi kuwa mradi huo ni muhimu na ni vema Serikali ikahakikisha utatekelezwa haraka. Akanihoji ni kwa nini ninaupinga?
Baada ya kunishawishi kwake nilimueleza kuwa hata mimi siupingi mradi huu, kwa sababu ni muhimu, lakini tatizo langu lipo kwenye namna unavyotekelezwa.
Baada ya kumwelewesha na kumwonyesha kwa mifano jinsi Serikali inavyokosea katika utekelezaji wa mradi huo, hatimaye tulikubaliana kuwa kuna mambo kadhaa yanayohitaji kurekebishwa ili mradi huu uwe na manufaa kwa umma na taifa kama inavyotarajiwa.
Kati ya mambo tuliyokubaliana na msomaji wangu huyo ni kuwa hadi hivi sasa, hakuna uhakika wa moja kwa moja unaoonyesha jinsi wakazi wa Kigamboni wa sasa watakavyonufaika na mradi huo.
Msomaji wangu huyo na mimi tulikubaliana kuwa pamoja na mradi kuwa na manufaa makubwa kwa taifa, lakini watu watakaoathirika na mradi huo, kama vile wakazi wa maeneo yatakayotwaliwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, wanapaswa kunufaika pia.
Siyo siri kuwa kwa kiasi kikubwa mradi utajengwa na wawekezaji na kila mmoja anafahamu fika kuwa ni wachache sana kati ya wawekezaji hawa, kama watakuwepo, ambao watatoka hapa nchini.
Mtu yeyote anapowekeza, lengo lake kuu la kwanza ni kupata faida kutokana na uwekezaji wake. Kwa kuwa wawekezaji hawa kutoka nje ndiyo watakaotoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwekeza, basi na sehemu kubwa ya faida itakwenda kwao.
Serikali itabakia kupata kiasi kidogo cha kodi na ushuru (kama wawekezaji hawatapewa msamaha wa kodi).
Sasa kama Serikali yenyewe itabakia kupata fedha kidogo kupitia kodi huku sehemu kubwa ya faida ikienda kwa wawekezaji, ni nani atamtetea mwananchi mnyonge ambaye leo hii anaondolewa katika eneo lake ili kupisha mradi huo.
Kwa kuhoji kwa nini Kigamboni isijengwe Dodoma sikumaanisha kuwa mradi huo wa Kigamboni usitekelezwe Kigamboni na badala yake utekelezwe Dodoma. Nilichokuwa nafanya ni kujaribu kukumbusha kuwa ipo miradi inayofanana na hiyo, kama ule wa ujenzi wa makao makuu Dodoma, ambao umekuwa kwenye makaratasi kwa zaidi ya miaka 30 sasa, lakini hakuna dalili za utekelezaji wake.
Miradi kama hiyo imechelewa wakati haina mawaa katika utaratibu wa utekelezaji wake. Inashangaza kuwa mradi huu wa Kigamboni umebuniwa katika miaka ya hivi karibuni, lakini kasi yake ya utekelezaji inaonekana kuwa kubwa ajabu.
Tofauti baina ya miradi hii miwili ni kuwa ule wa Dodoma unapaswa kutekelezwa na Serikali, wakati huu wa Kigamboni una mkono wa wawekezaji.
Kwa umuhimu kama nchi, mradi wa Dodoma una maana kubwa kuliko huu wa Kigamboni. Lakini inashangaza kuwa Kigamboni inapewa kipaumbele zaidi ya Dodoma. Ni rahisi kuhisi hapa kuwa kuna mkono wa wawekezaji nyuma ya kasi hii ya kutaka kuwahamisha watu bila kufuata utaratibu ili lipatikane eneo la wawekezaji kutengeneza fedha zao.
Jambo jingine lianaloonyesha shinikizo la wawekezaji nyuma ya mradi huu ni jinsi Serikali ilivyoamua kuziweka kando sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa mradi wenyewe.
Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile ameeleza vema kwenye moja ya taarifa zake.
Mbunge huyo anaeleza kuwa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, walipokutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hivi karibuni ili kuujadili mradi huo pamoja na maofisa wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilibainika kuwa sheria, kanuni na taratibu nyingi zinazohusu kubadili matumizi ya ardhi ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huu hazikuzingatiwa na kufuatwa kikamilifu.
Ilibainika pia kuwa ushirikishwaji wa kina wa wananchi, ambao ardhi yao imepangwa kutwaliwa kwa ajili ya mradi huu haukufanyika. Wao wamekuwa wakipokea amri na maagizo kutoka ngazi za juu ambayo wanatakiwa kuyatekeleza.
Ilibainika kuwa halmashauri na Serikali za mitaa husika, ambamo eneo linalotwaliwa zimo, hawakuhusishwa.
Lakini, wizara imeenda mbali zaidi na kuunda mamlaka nyingine, Kigamboni Development Authority (KDA), ambayo itakuwa na mamlaka ya uendeshaji wa mji mpya wa Kigamboni bila kujali kuwa mamlaka hiyo imeundwa ndani ya mamlaka nyingine, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, ambayo haikuhusishwa katika utaratibu wa uanzishwaji wa mamlaka mpya.
Mchakato huu unatawaliwa na sheria tano ikiwa ni pamoja na Sheria ya Utwaaji Ardhi namba 47 ya mwaka 1967; Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya 2007; Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999; Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997 na Sheria ya Serikali ya Mitaa namba 8 ya 1982.
Hadi hivi sasa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekiuka sheria hizi katika utekelezaji wa mradi huu. Sielewi, baada ya kukiuka sheria zote hizi tano, wizara inapata wapi mamlaka ya kushinikiza mradi uendelee.
Akionyesha kutoshirikishwa kwa wananchi, Dk. Ndugulile anasema: “Watendaji wa Wizara wamekuwa hawafuati sheria na badala yake wamekuwa wakitumia ubabe, nguvu na usiri mkubwa katika utendaji kazi wao.
“Aidha, wananchi wamekuwa wakitaarifiwa na siyo kushirikishwa katika mchakato wa mradi huu. Kuna tofauti kubwa kati ya kutaarifu na kushirikisha.”
Hata kama changamoto zitatatuliwa na mradi kuendelea, katika mazingira kama hayo, hivi bado Wizara inataka tuiamini katika utekelezaji wa mradi huu?
Kama kweli kuna dhamira ya dhati, isiyo na chembe ya shinikizo kutoka upande wowote, Wizara haina budi kuhakikisha kuwa mchakato wa mradi huu unaanza upya.
Na hilo ndilo liliagizwa kwenye kikao cha Waziri Mkuu, Wabunge na maofisa wa Wizara.
Lakini, hivi ni jambo la busara kweli kuwaamini wale wale ambao walituburuta awali na kukiuka sheria, kanuni na taratibu, warudie tena kuufanya mradi huu?
Hivi tukiwaamini hawa hawa tutarajie matokeo mengine tofauti na tulichokishuhudia?
Ndiyo maana nikapendekeza katika makala yangu ya kwanza kuwa ni vema tukaelekeza nguvu kwenye mradi wa makao makuu Dodoma, ambayo itawanufaisha Watanzania moja kwa moja kuliko kujihangaisha ya Kigamboni ambayo inashinikizwa na wawekezaji kwa ajili ya faida zao.